
ZANZIBAR ELECTRICITY CORPORATION
(ZECO)



WITO umetolewa wa kusimamia na kutekeleza miradi kwa kasi na ufanisi ili iweze kutoa tija kwa wakati stahiki kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar, Ndugu: Joseph John Kilangi ameyasema hayo kabla ya kutiwa saini kwa Mkataba wa matengenezo na uimarishaji miundo mbinu ya umeme eneo la mji wa Zanzibar katika hafla iliyofanyika ofisi za Wizara Maisara, Mjini Unguja.
Katibu Kilangi amewataka watendaji wa Wizara na Idara zilizo ndani ya Wizara hiyo kuwasimamia wakandarasi wa mradi huo kutekeleza kwa wakati.
Hata hivyo, ameitaka kampuni iliyopewa kazi hiyo kuitekeleza kwa ufanisi ili waweze kupatiwa kazi nyengine za miradi ya umeme inayotarajiwa kutekelezwa na Wizara hiyo badala ya kupewa kampuni za nchi za nje.
Naye Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi: Haji Haji alisema kuwa mradi huu ni miongoni mwa hatua za uimarishaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambapo utajenga vituo viwili vya kupokea na kusambazia umeme pamoja na ujenzi wa njia (33kV) za kusafirishia umeme.
Alieleza kuwa kwasasa njia za kusafirisha umeme ndani ya mji wa Zanzibar zina uwezo wa kubeba Kilovolti 11kV ambapo kupitia mradi huu njia zenye uwezo wa kilovolti 33kV zitajengwa eneo la mjini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Kampuni ya Central Electricals International Limited ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuutekeleza mradi huo kwa ufanisi wa hali ya juuu. Aidha, ameithibitishia Wizara kuchukuwa Wazanzibari katika kutekeleza kazi za mradi huo.
Mradi huo wa uimarishaji miundo mbinu ya umeme ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ZESTA (Mradi wa Uimarishaji Sekta ya Nishati na Upatikanaji wa Huduma ya Umeme Zanzibar) ambapo mbali na kujenga vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme kwa kutumia nishati ya jua, kujenga njia (132kV) za kusafirisha umeme na kuwaungia wananchi umeme, kuimarisha miundo mbinu ya Mji Mkongwe ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huu.
Sehemu hii ya utekelezaji wa mradi huu itagharimu dola za Marekani milioni 17.2 USD ambapo utahusisha ujenzi wa vituo vya umeme pamoja na kujenga mfumo wa usafirishaji umeme ndani ya Mji Mkongwe.