Kuunganishwa na huduma ya umeme ni rahisi mno. Unachohitajika ni kufuata hatua chache tu na utakuwa tayari kun’gara!


Hatua ya 1: Kuweka mfumo wa umeme

Kabla ya kufika ZECO kwa ajili ya kusajiliwa kwa ajili ya kuunganishwa na umeme, kwanza unahitaji kuhakikisha kuwa nyumba/jengo lako limefanyiwa mfumo wa umeme (fitting) uliojumuisha main switch. Mfumo wa umeme ni lazima ufanywe na mkandarasi au fundi mwenye sifa.

Hatua ya 2: Usajili

Usajili unafanyika katika makao makuu Gulioni Unguja na Tibirinzi kwa wateja wanaoishi Pemba, na pia katika ofisi zetu za kanda Unguja na Pemba. Usajili utafanywa na mmiliki wa jingo tu vinginevyo hati ya uwakala (power of attorney) itahitajika kwa mtu atakaemuwakilisha mmiliki.

Ili kusajiliwa unahitaji kuwasilisha picha moja ya pasipoti na kitambulisho halali chenye picha kinachokubalika (Kitambulisho cha Mzanzibari, Kitambulisho cha Mtanzania, leseni ya udereva, pasi ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura)

Afisa husika ataingiza taarifa zako ndani ya mtandao wa kompyuta na fomu ya usajili itachapishwa kwa ajili ya kufanyia malipo. Aidha utapewa maelezo yote juu ya masharti ya kuunganishiwa umeme.

Utatakiwa kulipia ada ya usajili. Ikiwa utahitaji kutumia transfoma yako pekeyako, utalazimika kufanya maombi mbali kwa Meneja Mkuu.

Hatua ya 3: Upimaji

Afisa husika wa ZECO atawasiliana na wewe kukupa taarifa ya lini watakuwa tayari kuja kufanya upimaji katia eneo lako.

Baada ya kufanyiwa upimaji utapewa taarifa ya gharama za kuunganishiwa umeme, na utatakiwa kulipa gharama hizo. Hakikisha umepata na kuitunza stakbadhi ya malipo hayo.

Hatua ya 4: Kuunganishiwa umeme

Baada ya kufanya malipo ya kuunganishiwa umeme, maafisa wetu watawasiliana nawe kukupa taarifa ya lini watakuwa tayari kukuunganishia umeme katika jengo yako.

Hatua ya 5: Furahia maisha yenye kung'ara!

Sasa uko tayari kuanza maisha yenye kung’ara. Tafadhali usisahau kuhifadhi matumizi ya umeme ili kulinda mazingira na dunia yetu! Aidha usisahau kulipia bili zako ili kuepusha usumbufu wa kukatiwa umeme!