Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) ni shirika pekee la uzalishaji na usambazaji umeme Zanzibar. Huduma zetu zinagusa nyanja zote za usambazaji wa umeme, kuanzia usajili , usambazaji hadi kufunga mita kwa wateja wetu. Makadirio ya gharama za uingizaji umeme zinatofautiana kulingana na masafa ya alipo mteja kutoka kwenye nguzo pamoja na vifaa vinavyotumika kulingana na makadirio yatakayopangwa na maafisa tathmini wetu.

Kwa kuwa dhamira yetu ni kusambaza umeme kwa watu na sekta zote, tumezigawa huduma zetu katika viwango tofauti vya matumizi ikiwemo watumiaji wa majumbani, biashara ndogondogo, biashara na viwanda vikubwa, pamoja na kuunga umeme wa muda kwa mujibu wa mahitaji ya wateja wetu wote.

Kuhifadhi miundombinu na huduma zetu ni jukumu letu sote. Hivyo basi ni kosa la jinai kujihusisha na vitendo vyovyote vya ubadhirifu ikiwemo kuunganisha umeme bila ruhusa ya shirika. Hukumu ya mtu anaebainika kuunga umeme kinyume na taratibu ni faini isiyopungua Shilingi Milioni Moja au kwenda jela kwa muda usiozidi miezi sita au yote mawili, pamoja na kulipa gharama za matumizi ya umeme katikakipindi chote ambacho amefanya udanganyifu huo.