ZECO YATAKIWA KUBORESHA HUDUMA 

Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) limeshauriwa kuboresha huduma zake zaidi katika eneo la huduma za dharura ili kupunguza malalamiko kwa wateja wake.

Wakichangia ripoti iliyowasilishwa na Meneja Mkuu Shirika la Umeme Zanzibar juu ya utendaji wa Shirika hilo kwa mwezi Julai hadi Disemba 2020, wajumbe wa kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi katika afisi za Shirika zilizopo Gulioni Zanzibar wamesema kuwa licha ya Shirika kupiga hatua kubwa za usambazaji umeme pamoja na uimarishaji wa miundo mbinu ya umeme mapungufu yaliyobakia kwa Shirika ni kuchelewa kutatua matatizo kwa uharaka.

Wamesema kuwa kuboreka kwa huduma za umeme nchini kutapelekea kukuza uchumi wa nchi na hata kuongeza mapato ya Shirika jambo ambalo litapelekea Shirika hilo kuongeza gawio Serikalini.

Akijibu hoja zilizotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo Meneja Mkuu Shirika la Umeme Zanzibar Mhandisi Hassan Ali Mbarouk amesema kuwa Shirika hilo limejipanga vya kutosha ili kuweza kuwahudumia wateja wake na siku chache zijazo Shirika litapokea gari mpya kwa ajili ya kuboresha huduma za dharura.

Amesema kuwa tatizo la uwepo umeme mdogo kwa baadhi ya maeneo husababishwa na kuzidiwa kwa miundo mbinu ya umeme aidha kimatumizi kwa wateja wake au ujenzi wa miundo mbinu ya umeme usioridhisha unaotokana na kutumia mafundi wa nje ya Shirika.

Akifafanua kuhusu uwezo wa Shirika wa kutoa gawio Serikalini amesema kuwa kwa muda wa miaka mitatu sasa Shirika limeweza kupeleka gawio na limekua likiongezeka kila mwaka kulinganisha na zamani ambapo lilianza na kutoa gawio la Shilingi milioni mia mbili (200) hivi sasa kufikia hadi bilioni.

Wakati akiwasilisha ripoti ya utekelezaji ya Shirika la Umeme (ZECO) Meneja Mkuu amesema kuwa hadi kufikia mwezi Disemba 2020 Shirika linadai kiasi cha shilingi bilioni 44.4 kwa wateja wake wakubwa na deni hilo linaongezeka kutokana na kuendelea kutumia mita za zamani kwasababu matumizi yao hayahimili mita za TUKUZA.

Aidha amefafanua kuwa watumiaji wadogo wote wameshabadilishiwa mita na kufungiwa mita za TUKUZA jambo lililopelekea Shirika hilo kuongeza ukusanyaji wake wa mapato isipokuwa ubadilishaji wa mita unaoendelea sasa ni baina ya mita za TUKUZA za zamani na kuweka mpya.

Ameongezea kuwa Shirika limekua likichukua hatua mbali mbali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya umeme kwa kufanya kazi ya kubadilisha nguzo mbovu kwa kila wiki, kusawazisha maeneo yenye umeme mdogo, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa transfoma na ubadilishaji wa taransfoma zisizohimili matumizi kwa wateja.

Ziara ya Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi inayoongozwa na Mhe. Panya Ali Abdalla imefika kwa mara ya kwanza Shirika la Umeme Zanzibar tokea kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Mbali na kupokea ripoti ya utekelezaji wa Shirika hilo kwa mwezi wa Julai-Disemba, 2020 kamati hiyo pia ilitembelea kituo cha kupokelea umeme Fumba na kujionea athari za mazingira pembezoni mwa kituo cha umeme Fumba.