Nishati mbadala yatajwa kuwa chachu ya kuongeza mapato Zanzibar

KATIKA utaratibu wake wa kukutana na wafanyakazi Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) imefanya mkutano wake wa kawaida katika kujadili mambo mbali mbali yaliopo na changamoto zinazolikabili Shirika hilo.
 
"Tujitayarishe kusimama kwa miguu yetu, tunajaribu kulifanya Shirika liwe "competitive" siku za mbele au kuwa "financial sound". Amesema.
 
Akifafanua juu ya jitihada mbali mbali walizochukua kuwa ni pamoja na kuandaa mapendekezo ya miradi mbali mbali ikiwemo mpango wa ujenzi wa miundo mbinu kwa ajili ya uzalishaji nishati mbadala (jua) ya umeme yenye uwezo wa kutoa megawati 50 na ujenzi wa njia nyengine ya umeme wa baharini.
 
Amesema kuwa katika jitihada hizo nchi na mashirika mbali mbali wameweza kuwasiliana nayo juu ya adhima hizo ikiwemo Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), Shirika la Maendeleo la Sweeden (SIDA) pamoja na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na mashirika hayo yameonesha nia ya kushirikiana nao lakini janga la dunia la maradhi ya corona limekwamisha kufikia mafanikio hayo.
 
Aidha amebainisha kuwa endapo Shirika litafanikiwa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati hiyo ya jua asilimia kubwa ya mapato ya Shirika yataweza kutumika katika shughuli mbali mbali za uendeshaji na maendeleo ndani ya Zanzibar badala ya kutumika katika kununua umeme.
 
Kwa upande mwengine wafanyakazi wa Shirika la Umeme Zanzibar wamepongeza jitihada za bodi hiyo lakini wameshauri ushirikishwaji wa wafanyakazi katika mambo mbali mbali yanayowagusa wafanyakazi ili kuzidi kujenga imani baina ya wafanyakazi hao na uongozi.
 
Aidha, wamependekeza kuwa Shirika liongeze nguvu zaidi katika kuwahudumia wafanyakazi wanaopata ajili kazini ikiwezekana hata kuwasafirisha nje ya nchi ili kuepusha na madhara ya ulemavu wa maisha.
 
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar pamoja na Menejimenti ya Shirika huwa na utaratibu wa kukutana na wafanyakazi mara kwa mara katika kuelezea hatua na mafanikio mbali mbali yaliyofikiwa katika kuliendeleza Shirika.