Wafanyakazi watakiwa kujiepusha na mgongano wa kimaslahi katika majukumu ya kazi zao

WAFANYAKAZI wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) wametakiwa kufanya kazi kwa maslahi ya Shirika na kuacha majungu ili kulipeleka mbele Shirika hilo.

Akizungumza na wafanya kazi wa Shirika hilo katika ofisi za Shirika la Umeme Saateni ikiwa ni mara ya kwanza tokea kuteuliwa kwake, Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Mhandisi; Mshenga Haidar Mshenga amesema kuwa ni lazima wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii ili kuliongezea tija Shirika.

Amewataka wafanyakazi hao kuweka mbele maslahi ya ZECO na si vyenginevyo kwani hilo ndio jambo la msingi lililomleta katika taasisi hiyo.

Amefahamisha kuwa baadhi ya wafanyakazi wanatabia ya kubaguana kwa msingi wa maeneo na makundi hivyo amewataka kuacha tabia hiyo kwani ni dalili ya kulirejesha nyuma Shirika kimaendeleo.

Mhandisi; Mshenga amefafanua kuwa licha ya uwepo wa malalamiko mengi kwa wafanyakazi lakini amewataka kufanya kazi kwa juhudi, maarifa, utii, upendo na uvumilivu ili kuliongezea tija Shirika kwani jamii na taifa linategemea wafanyakazi hao katika kuwapatia huduma bora.

Amewatahadharisha wafanyakazi kuacha kuchanganya baina ya maslahi binafsi na ya Shirika na hatamfumbia macho mtendaji atakayeshindwa kudhibiti matamanio yake na kulitia hasara Shirika kwa kuendekeza mgongano wa kimaslahi.

Mapema wafanyakazi wa Shirika hilo wamemuomba Meneja Mkuu huyo kufuatilia maslahi yao kwani maslahi ni jambo pekee linaloweza kumpatia mfanya kazi ari ya utendaji kazi.

Wamesema kuwa muongozo wa mishahara uliotayarishwa kwa ajili ya Shirika hilo umeacha athari kwa baadhi ya wafanyakazi kwani umepelekea baadhi ya wafanyakazi kuathirika mishahara yao.

Aidha, wafanyakazi hao wamemuomba Meneja huyo kuwashirikisha wafanyakazi katika kila jambo linalohusu maslahi ya wafanyakazi kwani miongozo mingi inayotungwa wafanyakazi wa chini ndio wanaoathirika.

Wamefahamisha kuwa licha ya wingi wa wafanya kazi katika Shirika hilo Meneja Mkuu ameshauriwa kuwatumia wawakilishi wa vyama mbali mbali vya wafanyakazi kama vile TUICO ili kuepusha mivutano kwa baadhi ya miongozo inayopitishwa na kutumika.

Mkutano huo ni wa kwanza kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika hilo kwa Meneja Mkuu huyo tangu ateuliwe na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kushika nafasi hiyo ya umeneja mkuu tarehe 4 Mei, 2021.