Wananchi wa kijiji cha Kidagoni wametakiwa kufuata utaratibu wa kujiungia umeme kupitia vituo vya Shirika la Umeme badala ya kuwatumia watu katika kujipatia huduma ya umeme.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mawasiliano wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Haji Juma Chapa wakati wa ziara ya kutembelea na kujionea maendeleo ya kazi ya ujenzi na usambazaji umeme kijini hapo.

Amefafanua kuwa baadhi ya watu wasio na nia njema hutumia fursa ya vijiji vipya kuwachukulia wananchi pesa kwa lengo la kuwapatia huduma ya umeme kwa bei nafuu jambo ambalo huwaweka wananchi katika wakati mgumu wa kupata huduma hiyo kutokana na kutofuata utaratibu.

Amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia njema ya kuwafikishia wananchi wake huduma zote za kijamii mijini na vijijini bila ya kujali gharama za upelekaji wa huduma hizo.

Ndugu Chapa amewataka wananchi wa kijiji hicho kuilinda miundo mbinu hiyo kwani gharama kubwa inatumika katika kuwapelekea wananchi hao huduma.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji hicho wamelishukuru Shirika la Umeme ZECO kwa kuwaona na kuwapelekea huduma hiyo ya umeme kwani itaweza kuinua hali zao za maisha na maendeleo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho wameeleza kuwa kijiji hicho kimekosa kuona na kujua mambo mbali mbali yanaoendelea hapa nchini na ulimwenguni jambo ambalo linawafanya kuwa nyuma kimaendeleo.

Akielezea baadhi ya mafanikio na matarajio ambayo wanayoweza kufaidika nayo mwalimu mkuu wa skuli ya Kidagoni Makame Juma Badili amefafanua kuwa uwepo wa huduma ya umeme kijijini hapo kutawasaidia wanafunzi wa skuli hiyo kuweza kujisomea hata nyakati za usiku na kuwaepusha na athari za matumizi ya taa zisizo salama.

Ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia taasisi zake na Chama cha Mapinduzi kwa kuwapatia misaada mbali mbali ya vifaa ikiwemo mashine za kuchapia karatasi na kompyuta lakini imewabidi kuviweka vifaa hivyo kwa mwalimu badala ya skulini hapo kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme katika skuli hiyo.

Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linakusudia kutumia kiasi cha shilingi milioni 101 hadi kukamilika kwa mradi huo.

Baadhi ya kazi zilizokwisha kamilika hadi sasa ni ujenzi wa laini ya umeme wa mkondo mkubwa yenye urefu wa kilomita 1.2km pamoja na kuwekwa transfoma yenye ukubwa wa 50kVA ambapo kazi iliyobakia hivi sasa ni ujenzi wa laini ndogo ya umeme yenye urefu wa kilomita 2km pamoja na kuwaunganishia wananchi.

Kijiji cha kidagoni kilichopo Shehia ya Kidoti Wilaya ya Kaskazini A Unguja kina wakaazi wasiopungua 200 ambapo hakijawahi kupata huduma ya nishati ya umeme.