ZECO yakusudia kutanua huduma zake mikoani

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) linakusudia kuimarisha huduma zake katika vituo vya mikoani ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma zake.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa ziara ya kutembelea vituo hivyo na kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa hapo siku za karibuni Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar

Mhandisi; Hassan Ali Mbarouk amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2021 kituo cha zoni ya Kaskazini Kilichopo Gamba na cha zoni ya Kusini kilichopo Makunduchi vitakua vinatoa huduma zote za umeme kama zinavyotolewa katika kituo kikuu.

Amefahamisha kuwa ingawaje asilimia kubwa ya maagizo aliyotoa yametekelezwa lakini bado baadhi ya huduma hazijakamilika ikiwemo pamoja na kuweka mazingira mazuri ya makaazi na matengenezo ya ofisi.
Amesema kuwa vituo hivyo vinakusudiwa kutoa huduma zote ambazo zinatolewa katika kituo kikuu cha ufundi Saateni zikiwemo utoaji wa huduma za kiufundi masaa 24 pamoja na kuwaungia wateja wapya.


“Tumekusudia viweze kujitegemea kwa kila kitu, kuwe kuna mafundi ambao watakuwa station (wanakaa) humu masaa yote na watakuwa wanaweza kufanya kazi kama zile ambazo zinafanywa katika kituo chetu cha ufundi pale Saateni. Vituo hivi vitakuwa vinajitegemea na vinafanya kazi zote na huo ndio mpango uliopo” alisema.
Katika maagizo ambayo aliyatoa kwa watendaji wake katika kufikia hatua hiyo ya kujitegemea kwa vituo hivyo ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa mfumo wa maji ambao umeshakamilika, ukarabati wa mapaa na maboresho ya ndani ambayo bado hayajakamilika.

Mbali na utekelezaji huo wafanyakazi wa kituo cha Makunduchi wameliomba Shirika kuzingatia hali ya usalama wa kituo kwa kujenga uzio ili kudhibiti mali za Shirika pamoja na wafanyakazi hao.
Vituo vya Gamba na Makundichi vilijengwa na Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume mwishoni mwa miaka ya 1960 ujenzi ulioenda sambamba na nyumba za maendeleo.


Kutokana na uchakavu wa miundo mbinu yake vituo hivyo vilisita kutoa huduma mnamo miaka ya 1980 lakini virejea tena kutoa huduma zake Januari 2013 kwa kuanzia na huduma za uuzaji wa umeme pamoja na huduma za dharura katika zoni ya Kusini na Kaskazini Unguja.