ZECO yakabidhi msaada wa kompyuta

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) limetoa msaada wa kompyuta moja kwa kituo cha Polisi Makadara kilichopo Mkoa Mjini Magharibi Unguja katika kusaidia ufanisi wa kazi zao na kujenga mahusiano

mazuri baina ya ZECO na jeshi hilo.

Akikabidhi kompyuta hiyo Meneja Mkuu Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi; Hassan Ali Mbarouk amesema kuwa kitendea kazi hicho ingawaje ni kimoja kwa kuanzia lakini kitasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi zao.

Aidha ameshukuru watendaji wa kituo hicho kwa mahusiano yao mazuri na ya karibu baina yao na uongozi wa Shirika la Umeme ikiwa ni pamoja na kupata ushauri katika jukumu la ulinzi na usalama wa Shirika.

Meneja Mbarouk amenasihi kuwa mahusiano mazuri baina ya jeshi hilo na jamii inayozunguuka kituo hicho ndio yatakayopelekea kuzidi kuimarisha amani ya nchi hivyo hayana budi kukuzwa na kuimarishwa.

Nae mkuu wa kituo hicho Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Maulid Kheir Maulid amelishukuru Shirika la Umeme Zanzibar kwa msaada wao huo ambao utaongeza kasi ya utendaji wa kazi zao.