ZECO YAFANIKISHA ILANI YA CCM

NA HUSNA MOHAMMED

NI miaka tisa sasa imetimia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwa chini ya uongozi wa Rais Dk, Ali Mohammed Shein tangu kuingia madarakani. Katika kipindi chake cha uongozi Rais Shein

ametekeleza huduma nyingi za kijamii kupitia ilani ya CCM kiasi kwamba leo hii amekuwa akipigiwa mfano hata na wapinzani.

Katika Makala haya tunazungumzia namna ya sekta ya nishati ilivyopiga hatua katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini Unguja na Pemba n ahata sehemu za visiwa vidogovidogo ndani ya visiwa hivi vikubwa vya Unguja na Pemba.

Ni wazi kuwa ndani ya kipindi cha miaka tisa ya uongozi wa Dk Shein, usambazaji na upatikanaji wa umeme katika visiwa hivi ni ya kupigiwa mfano kiasi kwamba malengo ya ilani ya CCM yamepitiliza kwa kuwa tayari umeme umefika karibu maeneo yote ya visiwa hivi.

Katika ibara ya 96A (i), ilani ya CCM iliagiza: “Kusimamia utekelezaji wa Sera na Sheria ya Nishati ya Mwaka 2009 na kuendeleza juhudi za upatikanaji wa umeme na nishati mbadala.” 

Aidha Katika ibara ya 96A (ii), CCM katika ilani iliagiza: “Kuimarisha shughuli za usimamizi wa huduma za umeme na usambazaji wa nishati hiyo mijini na vijijini vikiwemo visiwa vidogo vidogo vinavyoishi watu.

Ibara ya 96A (iii), inaelekeza kuwa: “Kuimarisha Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa lengo la kuliwezesha kujiendesha kibiashara.” Katika utekelezaji wa hili, jumla ya shilingi milioni 4.49 zimetumika kwa lengo la kuiwezesha ZECO kujiendesha kibiashara ili liweze kuleta faida stahiki kwa wananchi pamoja na serikali.  

Ili kuweza kujiendesha kwa ZECO kutaendana sambamba na sera ya serikali ya kutaka mashirika kuweza kujiendesha ili kuipunguzia mzigo serikali ili gharama zikiwemo za uendeshaji zilizopangwa kutumika hapo ziweze kutumika katika sehemu nyengine za jamii.

Aidha Katika kuhakikisha huduma bora, ZECO inaendelea na kazi ya kubadilisha mita za kawaida zote na kuweka mita za TUKUZA pamoja na kufunga mita kwa wateja wapya ili kujiongezea mapato.

Kufanikiwa kwa hatua hii kutawezesha ZECO kufanya kazi kwa uhakika na kudhibiti mianya ya mapato ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa ikitumika na wajanja katika kujikusanyia mapato.

Aidha, Shirika linaendea utekelezaji wa mpango wa mageuzi ili liweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja na kutoa tija kwa Serikali.

Kutokana na mageuzi haya. Shirika limeanza kupeleka gawio serikalini hadi kufikia shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka.

Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Rais wetu mpendwa Dk, Ali Mohammed Shein kwa kuwa na nia thabiti ya kuendeleza vyema nchi pamoja na wananchi wake, ambapo hata baada ya kukamilika kwa kipindi chake cha uongozi tutaendelea kumkumbuka daima milele kutokana na kuifanya sekta ya nishati kuenea maeneo yote.

Dk Shein, ni kiongozi wa awamu ya saba anaestahiki kupigiwa mfano hasa kwa azma yake ya kuviwezesha visiwa vidogo vidogo kupata umeme wa uhakika dhamira ambayo aliiweka chini ya ilani ya CCM wakati akiomba ridhaa za wananchi na hilo limefanikiwa kwa stahili yake.

Kwa kuzingatia dhana pana ya nishati na umuhimu wake katika maisha na kukuza maendeleo ya jamii na uchumi na kuongeza kasi ya uzalishaji Serikali imeendelea na juhudi za kusimamia na kuelimisha wananchi juu ya matumizi salama ya nishati tofauti nchini.

Sambamba na hilo, lakini katika kusimamia utekelezaji wa Sera na Sheria ya Nishati ya Mwaka 2009 na kuendeleza juhudi za upatikanaji wa umeme na nishati mbadala serikali imetekeleza ahadi ya kufikisha umeme karibu maeneo yote ya mijini na vijijini Unguja na Pemba.

Akizungumza na Makala haya, Meneja wa mawasiliano kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Salum Abdalla, juu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusiana na sekta ya nishati ya umeme Zanzibar, alisema kuwa serikali imetekeleza vyema ilani hiyo kwa sekta hiyo imevuka lengo jambo ambalo ni la kujivunia katika uongozi wa Dk Shein.

“Ama hili la nishati rais Shein ameitekeleza vyema ilani ya CCM kwa kuwa umeme sasa unang’ara hadi katika visiwa vidogovidogo jambo ambalo linafaa kupongezwa sana”, alisema Salum.

Akifafanua zaidi meneja mawasiliano huyo, alisema serikali imeimarisha shughuli za usimamizi wa huduma za umeme na usambazaji wa nishati hiyo mijini na vijijini vikiwemo visiwa vidogo vidogo vinavyoishi watu.

Salum alisema kuwa nishati ya umeme katika visiwa vya Unguja na Pemba imesambazwa kwa zaidi ya asilimia 90.

“Serikali imefanikiwa kusambaza umeme maeneo yote kwa zaidi ya asilimia 90 kazi iliyobaki ni kuwawezesha wananchi kujiungia na kuweza kuutumia umeme kwa maendeleo yao kwa vile fursa imeshafikiwa maeneo karibu yote ya visiwa hivi”, alisema.

Aidha alisema katika kuona tija inawafikia zaidi wakulima Serikali imeweza kufikisha huduma hizo hadi mabonde ya mpunga ili wakulima kupata fursa ya umwagiliaji.

Pia meneja huyo alisema ili kuona huduma za umeme zinawafikia watu wote, serikali imetoa fursa kwa wananchi kujiungia na itakapofika mwaka 2023 vijiji na maeneo mapya yawe yameshanea huduma ya nishati kwa maendeleo endelevu.

Hata hivyo, Salum alisema serikali chini ya uongozi wa Rais Shein, imeamua kuweka njia ya kuunga fursa ya umeme wa mkopo ili kuona wananchi wanafaidika na huduma hiyo muhimu ya kiuchumi.

“Lengo la serikali ni kuona kuwa shehia zote pamoja na vijiji zinafikiwa na huduma ya nishati na si hilo tu lakini wannachi wajiungie hata wale wasiokuwa na uwezo waweze kupata kwa mkopo hivyo wananchi watumie fursa hiyo”, alisema.

Sambamba na hilo, lakini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ZECO chini ya wataalamu wake inaendelea kazi ya ubadilishaji wa waya chakavu, nguzo mbovu pamoja na kukagua na kupima Transfoma Mijini na Vijijini kwa Unguja na Pemba.

Akizungumzia kuhusiana na usambazaji wa umeme katika visiwa vidogo vidogo, meneja huyo alisema katika kuhakikisha huduma ya Umeme inawafikia wananchi wote, serikali imeona umuhimu wa kuwafikishia wannachi wanaoishi katika visiwa vidogo ili waweze kunufaika na nishati hiyo muhimu ya kimaendeleo.

“Serikali imeshaanza maandalizi ya upelekaji Umeme kwenye visiwa vya Kokota na Njau huko ambapo ndani ya mwaka huu tunatarajia vipate nishati hiyo na kutimiza lengo la ilani ya CCM na ahadi ya Rais Shein wakati akiingia madarakani”, alisema.

Alisema usambazaji wa umeme katika visiwa vyote vidogo umefanywa kupitia wataalamu wa ZECO.

Aidha, Shirika limeshaanza utekelezaji wa mpango wa mageuzi ili liweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja na kutoa tija kwa Serikali.

Awali maendeleo ya sekta ya umeme Zanzibar yalianza kuimarika mnamo karne ya 20 ambapo majenereta ya mwanzo yaliyokuwa yakizalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe yaliwekwa katika kisiwa cha Unguja mnamo mwaka wa 1908.

Majenereta hayo yalifikia ukomo wa matumizi mwaka 1954 ambapo majenereta yaliyokuwa yakitumia mafuta mazito (diesel) yalifungwa na kutumika hadi mwaka 1980.

Katika mwaka huo wa 1980 kisiwa cha Unguja kiliunganishwa na Gridi ya Taifa kupitia mkondo wa umeme wa 132kV kwa kutumia waya wa chini ya bahari wenye uwezo wa kuchukua megawati 45MW.

Kutokana na uchakavu wa waya huo, mnamo miaka ya 2013 waya mwengine mpya wa chini ya bahari uliwekwa wenye uwezo wa kuchukua megawati 100MW kupitia mkondo wa umeme wa 132kV ambao unatumika hivi sasa.

Kwa upande wa kisiwa cha Pemba, nishati ya umeme ilianza kutumika mnamo mwaka wa 1958 kwa kujengwa kituo kikuu cha umeme Tibirinzi.

Kutokana na mahitaji ya umeme kuongezeka kisiwani Pemba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanikisha ujenzi wa kituo kipya cha umeme huko Wesha.

Aidha Kituo cha Tibirinzi kipya cha Wesha kilianza kutumika mnamo mwaka wa 1985 kwa kufungwa majenereta matatu ya mafuta mazito (diesel).

Majenereta hayo yalikuwa na uwezo wa kutoa umeme wa megawati 1.5MW ambapo kuanza kutumika kwake kulipeleka kutotumika kwa kituo cha Tibirinzi.

Kwa sasa kisiwa cha Pemba kinatumia umeme wa 33kV kwa kutumia waya wa baharini wenye uwezo wa megawati 20MW uliounganishwa na gridi ya taifa kutoka Pangani Tanga kupitia Majani Mapana hadi Ras Mkumbuu – Pemba.

Awali Shirika la Mafuta na Nguvu za Umeme (SFPC) lilianzishwa mwaka wa 1964 chini ya iliyokuwa Wizara ya Maji, Ujenzi, Ardhi na Mazingira kwa Sheria nambari 12 ya mwaka 1964.

Sambamba na hilo, lakini Sekta ya umeme ilifanyiwa mabadiliko kwa mara nyengine tena mabadiliko ambayo yameiondosha Shirika la Mafuta na Nguvu za Umeme mnamo mwaka wa 2006 na kuanzishwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) katika kusimamia shughuli zote zinazohusiana na nishati ya umeme Zanzibar kwenye kuzalisha, kusambaza na kugawa umeme katika visiwa vya Zanzibar.

Pia Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ambayo ni msimamizi mkuu wa shughuli zote.

Kwa mukhtaza huo basi Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka tisa ya uongozi wa Rais Dk Ali Mohamed Shein, Shirika hilo limepiga hatua kubwa katika kuwafikishia wananchi wa visiwa hivi nishati ya umeme kiasi kwamba ilani ya CCM katika taasisi hiii imetekelezwa karibu asilimia 130.

Na kwa uungwana wake Rais wetu mpendwa Dk Ali Mohamed Shein kwa kuwa ahadi ni deni naye ameweza kulilipa deni hilo kwa wananchi aliowaahidi kiasi kwamba kila pembe ya visiwa hivi vinang’ara kwa kupatikana huduma ya umeme.